Ijuwe Sheria ya Haki Miliki Tanzania,  na Professor Alex Perullo

 Professor of African Studies and Ethnomusicology,

Bryant University

 Sheria ya Hakimiliki ni Nini?

             Sheria ya hakimiliki inalinda haki za watunzi, kama watunzi wa muziki, watunzi wa vitabu na wachoraji, ambao wametengeneza kazi halisi za muziki, kisanii, kimaandishi au kisayansi. Mara baada ya mtu kubuni kazi halisi, analindwa na sheria ya hakimiliki na yeye anamiliki kazi hiyo, halafu anaweza kuamua jinsi itakavyotumika. Hata kama mtunzi hajaandikisha kazi yake, atalindwa na sheria. Mtunzi anaweza kujisikia vizuri kwa kujua utunzi wa kazi zake unalindwa na atafaidika kimapato na haki za msingi kwa kazi zake. Hii inaitwa haki za kiuchumi na haki za msingi.

Nini Maana ya Kazi Halisi?

 

Umuhimu wa sheria ya hakimiliki ni wazo la kazi halisi. Kazi zote zilizotegenezwa na watunzi ni lazima ziwe halisi ili ziweze kulindwa na hakimiliki. Uhalisi kwa maana kwamba mtunzi anatengeneza kazi kwa kujitegemea ambayo ni tofauti kutoka kazi nyingine. Uhalisi ni moja ya sehemu zenye utata katika sheria hii ya hakimiliki kwa sababu siyo njia rahisi kugundua kazi halisi na isiyo halisi.

Ili kufahamu kwamba kazi ni halisi au siyo halisi, kuna maswali mawili ya kuuliza:

1) Kazi hiyo imetungwa kwa kujitengemea na

2) kuna ubunifu halisi wa kutosha? Kazi itakubalika ikiwa mtunzi hajaiga kutoka kazi nyingine.

Kwa mfano, kama mtunzi wa taarab anaandika wimbo bila ya kutumia ala za muziki au maneno ya watunzi wengine, atakuwa ametengeneza kazi halisi. Lakini, kama mtunzi wa taarab atatumia maneno au ala za muziki ya mtu mwingine, hatatetewa na sheria ya hakimiliki kwa sababu ametumia kazi ya mtu mwingine bila ya ruksa yake. Kwa upande mwingine, kama watunzi wawili wanatunga wimbo mmoja unaofanana, watunzi wote wanatetewa na sheria ya hakimiliki (hii haitokei mara nyingi).

Swali la pili, kama kuna ubunifu halisi wa kutosha, ni ngumu zaidi kuliko swali la kwanza. Ni lazima mtunzi aonyeshe kwamba kazi yake ina utofauti, hata kidogo na kazi nyingine. Kwa mfano, kama kikundi cha ngoma kinaandika wimbo mpya uliobebea vionjo vya kizamani, hiyo nyimbo mpya ni lazima iwe ina tofauti ya kutosha na ya zamani. Ni wazi kwamba haiwezekaniki kuelezea tofauti iliopo katika ngoma ya zamani na mpya, lakini ukisikiliza utaweza kutofautisha.

Wasanii wa kufokafoka (rap) wana hali pekee kwamba wanatumia vionjo vya watu wengine ndani ya muziki yao (inaitwa “sampling” kwa kiingereza). Ili kuweza kutumia hivyo vionjo vya watu wengine, wasanii wanahitaji kupata ruksa kutoka kwa mtunzi wa nyimbo au mtu anayemiliki ile nyimbo. Kwa hali ya Tanzania, mtu anayemiliki nyimbo mara nyingi ni wauzaji wa kanda, watayarishaji wa muziki wa kanda, au watunzi wenyewe.

 Kazi Inakamilikaje?

            Mpaka hapa, tumeona kwamba mtunzi anayetunga kazi halisi analindwa na hakimiliki. Licha ya uhalisi, ni lazima kazi ikamilike kwa uhakika na kuhifadhiwa ili iweze kulindwa. Hii ina maana kwamba mtunzi ambaye anatengenza kazi halisi anahitaji kuhifadhi kazi yake katika vihifadhi, kama karatasi, kanda au kanda za video ambavyo havitaweza kupotea kwa kipindi kifupi. 

Kwa watunzi wengi, hili sio tatizo. Kwa mfano, mchoraji mara nyingi anatumia karatasi au turubai, akiwa anachora. Lakini, kwa mtunzi au mchezaji wa muziki, ni ngumu kuhifadhi kazi zao. Mara nyingi, watunzi wa Tanzania wanatunga nyimbo bila ya kuandika maneno au ala za muziki. Mwanamuziki, peke yake au katika kikundi, atacheza nyimbo zake katika maonyesho ya wazi au atazirekodi. Kama nyimbo zake zimerekodiwa, nyimbo zake zitakuwa zimefadhiwa kwenye vihifadhi madhubuti, kama kanda, CD, kanda ndogo (DAT), au minidisk. Lakini, kama kazi zinachezwa, bila ya kurekodiwa, nyimbo hizo zitakuwa hazijahifadhiwa katika vihifadhi visivyo madhubuti na hazitalindwa kama kazi nyingine, ila zitalindwa na sheria ya hakimiliki chini ya hakishiriki.

 Nani Anamiliki Kazi?

Mpaka sasa, mtunzi anayebuni kazi halisi na anayehifadhi kitu halisi, anakuwa mmiliki wa kazi. Lakini, katika hali mbalimbali, watunzi wengi wanabuni kazi fulani, sio mtunzi mmoja. Kwa mfano, kutunga nyimbo, mtu mmoja anatunga shairi na mwingine anashiriki kutunga muziki. Hao wasanii wote wanamiliki wimbo huu kwa sababu kila mtu ameshiriki katika kutunga. Hii inaitwa watunzi wa pamoja.  

Watunzi wa pamoja wanapata haki sawa za kumiliki kazi, hata kama kuna watunzi wengi. Kama kila mtu wa bendi kubwa anashiriki kuandika nyimbo—hata kama anaandika sehemu ndogo au fupi—kila mshiriki wa bendi hiyo ana haki ya kumiliki wimbo huu. Isipokuwa, kama mshiriki mmoja hatungi sehemu halisi (angalia sehemu ya juu kuhusu kazi halisi), hapa nyimbo haitatetewa na sheria ya hakimiliki mpaka sehemu hiyo imeondolewa au bendi imepata ruhusa kutumia sehemu hiyo.

Katika hali ambapo kampuni inamuajiri mtunzi, kazi yoyote itakayofanywa na mtunzi chini ya mahitaji ya kampuni, inakuwa haki ya kampuni. Kwa mfano, kampuni mbalimbali za Tanzania zimewajiri wanamuziki au bendi kutumbuiza na kupromoti kazi za kampuni. Kampuni zinamiliki nyimbo na kazi zozote zinazofanyiwa na wanamuziki wake, isipokuwa kuwe na mkataba unaosema tofauti.

 

Kibali Kinafanyaje Kazi?

 

            Mtunzi wa kazi halisi anaweza kumpa mtu mwingine kibali kutumia kazi yake. Hii ina maana kwamba mtunzi, katika mkataba, anaweza kumruhusu mtu mwingine kutumia kazi yake katika sababu maalum. Kwa mfano, kama Juma anataka kurekodi wimbo wa Bahati, Juma anahitaji kupata kibali kutoka kwa Bahati kitakachosema kwamba anaweza kurekodi wimbo huu kwa malipo fulani. Bahati anaweza kuamua kama anataka kumpa Juma kibali pekee au kibali kisicho pekee. Kibali pekee kinampa msanii fulani haki pekee ya kurekodi, kufanya maonyesho, au kitu kingine na kazi halisi ya mtunzi fulani. Kuendelea na mfano wa Bahati na Juma, kama Juma anapata kibali pekee kurekodi kazi ya Bahati, mtu mwingine, hata Bahati mwenyewe, hawezi kuirekodi ile kazi ambayo amempa Juma. Lakini, Bahati anaweza kutumia kazi yake katika maonyesho au kufanya marekebisho, au anaweza kumpa mtu fulani haki pekee kufanya hii, lakini wote hawawezi kurekodi kazi ya Bahati zaidi ya Juma. Kibali kisicho pekee kina maana kwamba kila mtu ambaye anapata kibali kutoka kwa mwenye kazi anaweza kutumia ile kazi. Kwa mfano, Bahati anaweza kutumia kazi yake hata kama amempa Juma, au mtu mwingine kibali. Kibali pekee au kibali sio pekee kinaisha kwa miaka kumi na tano baada ya mkataba wa awali. Pia, mtunzi anaweza kutoa kibali cha haki za kiuchumi katika kazi yake, lakini hawezi kutoa kibali cha haki za msingi.

                       

Kazi Inaingiliwaje?

           

Sheria ya hakimiliki inaingiliwa kama mtu anatumia kazi ya mtu mwingine bila ya ruksa. Kwa mfano, mwanamuziki anayetumia nyimbo ya mtunzi mwingine bila ruksa yake anakuwa anaingilia kazi halisi ya mtunzi. Pia, mtayarishaji wa muziki anayerekodi maonyesho ya msanii bila ya kumwuliza kwa ruksa anakuwa anaingilia haki za msanii.

 

Inakuwaje Kazi Inapoingiliwa?

 

Mtu yeyote anayedhulumiwa haki, ana njia mbalimbali kudai haki yake. Kwanza, anaweza kuzuia kuendelea kuingiliwa katika kazi yake. Kwa mfano, kama mfanyabiashara ananakili albamu ya mwanamuziki, kwa ushahidi, mwanamuziki huyo anaweza kufungua kesi kusimamisha kazi ya mfanyabiashara. Pili, mtu anayedhulumiwa anaweza kuomba malipo ya gharama yaliyotokana na kuingiliwa kazi yake. Kuendelea na mfano wa awali, kama mfanyabiashara ameuza kinyume cha sheria albamu ya mwanamuziki, mwanamuziki huyo anaweza kumdai faida zilizotokana na albamu yake. Mwanamuziki pia anaweza kusisitiza kwamba nakala zote za albamu yake ambazo zimerudufiwa zinaharibiwe. Halafu, mara chache, Sheria ya Hakimiliki ina ruhusu vifaa vyote vinavyotumika kurudufia viharibiwe. Hii ina maana kwamba mfanyabiashara anayerudufu albamu za wasanii bila ya ruksa, anaweza kupoteza vifaa vyake vyote alivyotumia kwenye kurudufia. 

            Adhabu nyingine katika Sheria ya Hakimiliki ni, kwa watu wanaovunja sheria kwa mara ya kwanza, wanapata faini isiozidi shilingi millioni tano au kifungo kisichozidi miakia mitano au adhabu zote. Kwa watu wanaozidi kukiuka, faini haiwezi kuzidi shilingi millioni kumi au kifungo kisochozidi miaka mitano.

 

Hitimisho

 

            Mpaka sasa, tumejaribu kufahamu sheria ya hakimiliki na jinsi inavyofanya kazi nchini Tanzania. Lakini, ni lazima wasomaji watambue kwamba kijitabu hiki kimejaribu kuelezea kwa kifupi tu na kuna vitu vingi zaidi vya kujifunza. Huko Ulaya, Marekani na sehemu nyingine, kuna vitabu vingi na makala nyingi zikielezea kuhusu sheria hii inavyofanya kazi. Sehemu kubwa ya fasihi hii imetokana na kesi za hakimiliki zilizoingia mahakamani. Kwa sababu kesi za hakimiliki chache ziliingia mahakamani nchini Tanzania, katika siku za mbele tutajifunza zaidi jinsi sheria hiyo itakavyofanya kazi.

 

 

Back to Home page